Propellerads

Tuesday, October 25, 2016

mpoma

MJUE MGOMBEA URAISI MAREKANI

PropelleradsMJUE MGOMBEA WA KITI CHA URAIS WA MAREKANI NA NINI TUNACHOWEZA KUJIFUNZA KATIKA UCHAGUZI WA URAIS NCHINI TANZANIA

DONALD TRUMP

Na Mwandishi Maalum

Wakati mdahalo wa pili wa wagombea wa chama cha Republican unasubiriwa kwa hamu usiku wa Jumatano tarehe 16 Septemba, ni vyema kuandika machache kuhusu mgombea Donald Trump ambaye anaendelea kuongoza kura za maoni katika kundi kubwa la wagombea wa chama cha Republican kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kuingia Ikulu ya Marekani mwishoni mwa mwaka kesho. Katika kuchambua harakati za Bwana Trump za kuusaka uongozi wa juu wa taifa la Marekani pia tumejaribu kuanisha nini ambacho Watanzania wanaweza kujifunza wakati huu ambapo kampeni za kuwania Urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania zimepamba moto.

Donald Trump na Edward Lowassa
Tungependa kuanza makala hii kwa kuwalinganisha Bwana Donald John Trump na Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa ambao wote  kwa sasa wanawania viti vya Urais wa Marekani na Tanzania. Ni dhahiri kwamba wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijiuliza, “Je, Edward Lowassa ndiye Donald Trump wa Tanzania?”

Bwana Trump ni mfanyabiashara na mwanasaisa wa Marekani ambaye ana sifa ya kuwa mmoja wa watu matajiri sana, kama alivyo Mh. Lowassa ambaye pia anasemekana kuwa Mtanzania mwenye utajiri mkubwa. Trump ni mmiliki mkubwa wa ardhi na majengo wakati Mh. Lowasaa anadai kwamba msingi mkubwa wa utajiri wake unatokana na kumiliki ardhi na mifugo mingi huko sehemu za Monduli.


Mara kadhaa Bwana Trump amejaribu kuwania kiti cha urais wa Marekani, kama ilivyo kwa Mh. Lowassa. Wote wamekaririwa wakisema kwamba wanataka kuwania uongozi wa ngazi ya juu katika nchi zao ili kusaidia kuleta neema na maisha bora kwa wanainchi wa nchi zao. Wanadai lengo lao ni kupata fursa ya kutumia vipaji vyao ambavyo vimewapa utajiri ili kuinua hali ya maisha na kutajirisha jamii zao!

Katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini Marekani Bwana Trump anawania uteuzi wa chama chenye viti vingi katika bunge la Marekani cha Republican. Lowassa alianza “safari yake ya matumaini” kwa kuwania uteuzi wa chama cha CCM ambacho pia kina viti vingi kwenye bunge la Tanzania. Bahati mbaya alitupwa kapuni kwenye mchujo wa chama hicho huko Dodoma.

Ingawa Bwana Trump anaongoza katika kura za maoni kwenye chama chake cha Republican lakini anaonekana hapendwi sana na viongozi wakuu wa chama chake ambao wanapendelea wagombea wengine. Mh. Lowassa vile vile alianza kuwania uteuzi wa kupeperusha bendera ya CCM ambako mbali na kuungwa mkono na wanachama wengi wa kawaida waliomdhani kwa wingi, lakini alichujwa na viongozi wakuu wa chama hicho ambao inasemekana walikuwa na mapenzi na wagombea wengine.

Awali, Bwana Trump alitishia kujitoa kwenye chama cha Republican na kusimama kama mgombea binafsi endapo atafanyiw amizengwe. Hali hiyo iliwapa kiwewe na wasiwasi viongozi wa chama cha Republican. Hivi karibuni Bwana Trump alitangaza kwamba atamuunga mkono mgombea ambaye atateuliwa na chama cha Republica, huku akisisitiza kuwa bila shaka mgombea huyo atakuwa ni yeye. Katiba ya Tanzania hairuhusu mgombea binafsi wa kiti cha Urais, kwa hiyo baada ya kuenguliwa kutoka kwenye kinyang’anyiro cha kuiwakilisha chama tawala cha CCM kwenye uchaguzi wa Rais, Mh. Lowassa alilazimika kujitoa CCM na kuingia kwenye chama cha upinzani CHADEMA na kupitia huko ameteuliwa kupeperusha bendera ya UKAWA ambao ni muungano wa vyama vine vikuu vya upinzani.

Wote wawili, Bwana Trump na Mh. Lowassa wanaweza kuelezewa kama watu wenye misimamo mikali na maamuzi magumu. Katika safari za kutimiza ndoto zao kibiashara na kisiasa, wamekumbana na misukosuko mingi migumu lakini mara nyingi wameibuka na kusonga mbele. Wote si wanasiasa mahiri au wazungumzaji wazuri sana kwenye majukwaa, lakini wanasifika kwa utendaji, ufuatiliaji na ufanikishaji wa dhamira zao. Wote ni watu wenye roho ngumu na jeuri ya kutokata tamaa kwa urahisi. Na bila shaka wote wawili wanajitambulisha kirahisi kwa muonekano wa nywele zao.

Nafasi ya Donald Trump katika Siasa za Marekani
Baada ya kutoa utangulizi huo, hebu tujaribu kuona kwa undani historia, nafasi na changamoto za Bwana Trump katika siasa za Marekani na nini Watanzania wanaweza kujifunza kutokana na hali hiyo.

Bwana Trump alizaliwa tarehe 14 Juni 1946 akiwa mmoja kati ya watoto watano wa Baba Fred Trump na Mama Mary Anne. Wazazi wote wawili wa Bwana Trump wana asili ya kihamiaji kutoka nje ya Marekani, mama akiwa mzaliwa wa Scotland na upande wa baba wakiwa wahamiaji kutoka Ujerumani.

Kielimu, Bwana Trump ana shahada ya kwanza ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylavania. Alianza kujiingiza katika mambo ya  biashara akiwa na umri mdogo akiongozwa na baba yake mzazi. Baada ya kuhitimu chuo kikuu  mwaka 1968, aliingia rasmi kwenye kampuni ya baba yake ya ujenzi, umiliki na uuzaji wa majumba.  Donald alipanda haraka haraka na kufikia mwaka 1971, akapewa uongozi wa juu wa kampuni hiyo. Baadaye alipanuwa wigo wa biashara na kujiingiza katika masuala ya utangazji na burudani. Pamoja na misukosuko kadhaa ya kibiashara aliyoipitia, hivi sasa Bwana Trump anakadiriwa kuwa na utajiri wa kiasi cha dola 4.1 bilioni, akipata mshahara wa dola 250 milioni kwa mwaka.

Kisiasa, Donald Trump amewahi kuwa mwanachama wa vyama vya Republican, Reform Party, Democratic na Independent. Ingawa huko nyuma alihama chama cha Republican mara tatu, kwa sasa anawania uteuzi wa chama cha Republican ili aweze kugombea kiti cha Urais wa Marekani.  

Ingawa uchaguzi wa Urais wa Marekani utafanyika mwezi Novemba mwakani, tayari kuna zaidi ya wagombea 15 ambao wanawania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama cha Repubican kwenye uchaguzi ujao. Kwa hivi sasa kura za maoni miongoni mwa wafuasi wa chama hicho zinamwonesha Bwana Trump akiongoza kundi la wagombea wote kwa alama nyingi. Anafuatiwa kwa karibu na mombea pekee Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, Daktari Bingwa wa mishipa ya fahamu Dr. Ben Carson.

Hata hivyo wachumbuzi wa masuala ya siasa za Marekani wanasema kampeni ya Bwana Trump inatoa changamoto kubwa kwa uongozi wa chama cha Republican ambao unaonekana kutompenda kuwa mgombea wake. Wanamuona Trump kama “mnoko” na “mchafuzi” wa nafasi ya chama hicho kushinda dhidi ya wapinzani wao wa Democtartic. Uongozi wa Republican ungependelea kusimamisha wagombea wengine wasio na utata mkubwa kama Jeb Bush, Marco Rubio, John Kasich au Scott Walker.

Tayari Bwana Trump amezusha mitafaruku mikubwa na misuguano kutokana na matamshi yake hasi dhidi ya wahamiaji wenye asili ya Kihispania (hususani kutoka Mexico) ambao alinukuliwa akiwaita wahalifu, majambazi, wauaji na wabakaji. Pia amekwaruzana na baadhi ya wanasiasa waandamizi wa chama hicho akiwemo Seneta John McCain na Graham Lindsey. Katika mdahalo wa kwanza ukiwapambanisha wagombea kumi kwenye ulingo mmoja, Bwana Trump alisakamwa vikali na wagombea wengine huku akitupiwa maswali magumu na muongozaji wa mdahalo huo, ambayo yasemekana yalilenga kumkata makali. Trump aliweza kujibu mapigo na kumtupia madongo mazito muongozaji wa mdahalo huo Bi. Megyn Kelly wa kituo cha Televisheni cha Fox ambacho kina uhusiano wa karibu na viongozi wakuu wa chama cha Republican. Hivi karibuni pia amekwaruza na mgombea pekee  wa kike Carly Fiorina, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa kampuni ya kubwa kompyuta ya Hewlett-Packard.

Tatizo kubwa la chama cha Republican ni kwamba ingawa hawampendi Bwana Trump, ni lazima wawe makini jinsi ya kumkabili, kwa vile mpaka sasa anaonyesha kupendwa na wanachama na watu wengi wa kawaida ambao wamechoshwa na uongo wa “wanasiasa wa ndani”  wa jiji la Washington. Kwa watu wa kawaida, Trump anaonekana kama mgombea tofauti anayesema kitu kutoka moyoni mwake, ambaye anasema ukweli hata kama unauma. Wanamuona Trump kama mtu ambaye ana pesa zake lakini anataka kusaidia watu wengine kwa dhati na hasukumwi kuwania kiti cha Urais kutokana na “njaa” zake au maslahi binafsi.

Trump amekuwa akitishia kwamba endapo viongozi wa chama cha Republican watamchezea mchezo wa rafu, angeweza kujitoa chama hicho na kusimama kama mgombea binafsi, hatua ambayo itakiweka chama cha Republican kwenye hali mbaya ya ushindani na mahasimu wao wa chama cha Democtratic. Ingawa amelegeza msimam huo hivikaribuni baada ya kuona anaendelea kuongoza, lakini watu wa karibu  wanaomfahamu Trump wanasema si ajabu akageuza kibao tena endapo ataona ameonewa au amepigwa “goli la mkono” kwa msemo mpya. Akisimama kama mgombea binafsi, Trump anaweza kuzigawa kura za wafuasi wa Republican na wale wasiokuwa na mapenzi na chama chochote (independents)  na hivyo kupelekea wapinzani wao wa chama cha Democratic kupata ushindi kirahisi.

Bila shaka kwa sasa Bwana Trump ameshikilia kura ya turufu na ndiyo maana viongozi waandamizi wa chama chake cha Republican wamekuwa wakimbembeleza na kumsihi asichukuwe uamuzi mgumu wa kutoka chama hicho. Hata baadhi ya wagombea wenzake wamepunguza mashambulizi dhidi yake wakihofia mtafaruku zaidi. Endapo Trump ataendelea kuongoza na hivyo kujihisi anastahili kuteuliwa kuwa mgombea halali wa chama hicho lakini wagombea wengine wakakataa kumuunga mkono, kama ambavyo baadhi ya wagombea wakiongozwa na Gavana wa zamani George Pataki tayari wamejitokeza, hali ya baadaye ya chama hicho inatia mashaka.

Haiyumkiniki wachambuzi wengi wanasema Bwana Trump anayo nafasi ndogo ya kushinda uteuzi wa chama chake cha Republican, achilia mbali uwezo wa kushinda kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu mwakani. Hata hivyo wanasema Trump ni mtu ambaye hawezi kubezwa kirahisi. Wakifanya makosa, Bwana Trump anaweza kusababisha chama cha Republican kipoteze nafasi ya kushinda kiti cha wa Urais na hata kuwanyima uongozi wa bunge la Marekani kwa kukosa idadi kubwa ya wabunge kutokana na baadhi ya wapiga kura kuamua kupiga kura za hasira dhidi ya chama hicho na viongozi waalioko madarakani.

Nini Watanzania wanaweza kujifunza
Tumalizie makala hii kwa kuangalia nini wapiga kura wa Tanzania wanaweza kujifunza kutokana na harakati za ugombea wa Bwana Donald Trump wa kiti cha Urais wa Marekani.

Kama tulivyoonyesha mwanzoni mwa makala hii, vipo vielelezo vingi vinavyomfananisha Bwana Donald Trump na Edward Lowassa katika mbio zinazoendelea za kuwania kiti cha Urais nchini Marekani na Tanzania. Baadhi ya mambo ambayo tunaweza kujifunza ni pamoja na haya yafuatayo:

Kwanza, katika medani za siasa, hakuna rafiki au adui wa kudumu. Malengo ya mwanasiasa siku zote ni kupata ushindi katika uongozi na kufikia malengo hayo kunahitaji mbinu na mikakati tofauti. Si vyema kutumia mbinu zile zile au kung’ang’aniza matakwa ya viongozi wachache ambao wakati mwingine yanakinzana na mtizamo au matarajio ya wafuasi au wanainchi wa kawaida walio wengi.
Pili, ingawa mazingira ya hizi nchi mbili ni tofauti, lakini ni vyema chama tawala cha CCM chenye viti vingi bungeni kwa sasa kikawa macho ili kisipoteze uwingi huo kwa kuendeleza kampeni ya kuandama, kumbeza na kujaribu kumchafua Lowassa ambaye alikataliwa CCM na kulazimika kwenda upande wa upinzani ambako amesimamishwa kama  mgombea wao. Kura za hasira na huruma kwa wafuasi wa Lowassa na watu wa kawaida tu zinaweza kuwatoa CCM kileleni katika Jumba Kuu huko Dodoma.
Tatu, ipo haja ya kubadili katiba ya nchi ili pamoja na maboresho mengine iweze kuruhusu mgombea binafsi wa kiti cha urais na pia miundo ya serikali za mseto au muungano wa vyama.  Endapo kungelikuwa na nafasi hiyo Edward Lowassa huenda asingelazimika kutoka CCM na kujiunga na chama kingine cha upinzani, labda angesimama kama mgombea binafsi, hali ambayo ingeiteteresha CCM kidogo, lakini isingewapa wapinzani matunda yote ya ufuasi wake.
Mwisho, ni muhimu kuendesha siasa za kistaarabu. Hata kama mnatofautiana kimtizamo, Watanzania bado ni watu wa taifa moja. Mpinzani wako kisiasa si adui, leo yuko kule kesho mnaweza kuwa naye huku.  Donald Trump amekuwa akifadhili wagombea wa vyama vyote vya Republican, Tea Party na Democratic, hata kama yeye si mgombea au mwanachama wa vyama hivyo kwa wakati huo.
Wanasiasa wa Marekani wanapingana hadharani lakini wanaendelea kuzungumza kirafiki na kibinafsi kwa kuheshimiana.  Hata baada ya kushindwa katika sanduku la kura, aliyeshindwa anampigia simu aliyeshinda kumpa pongezi hata kama amemng’oa kwenye kiti alichokuwa amekalia kwa muda mrefu!
Vyombo vya dola vyenye jukumu la kulinda amani na usalama havipashwi kujiingiza katika minyukano ya kisiasa na kamwe havitakiwi kuegemea upande mmoja dhidi ya mwingine. Hiyo ndiyo siri ya ukweli kwamba mara nyingi chaguzi za Marekani zinaendeshwa kwa hali ya utulivu, haki, amani na usalama.  
Tujifunze yaliyo mazuri kutoka katika mfumo wa wenzetu (tukiacha yale mabaya) ili na sisi tuweze kusonga mbele na kufanikisha uchaguzi ujao kwa haki, amani na usalama.
KUPATA KAZI POPOTE NCHINI BONYEZA 'HAPA' CHINI. Propellerads

mpoma

About mpoma

Author Description here.. Nulla sagittis convallis. Curabitur consequat. Quisque metus enim, venenatis fermentum, mollis in, porta et, nibh. Duis vulputate elit in elit. Mauris dictum libero id justo.

Subscribe to this Blog via Email :