VICHEKESHO vya makomediani maarufu Bongo, Mussa Yusuph ‘Kitale’ maarufu zaidi kama Mkude Simba na Stan Bakora ni tishio kwa sasa Bongo.
Pengine kinachowabeba zaidi ni staili yao ya kuchekesha ya kujibizana. Kabla ya kujulikana kuwa Mkude Simba ndiye Kitale, komediani wa muda mrefu ambaye amepaishwa na staili yake ya uteja, watu walijua ni ujio wa wasanii wapya kwenye vichekesho.
Ukweli ni kwamba, ulikuwa ujio wa staili mpya ya msanii Kitale, lakini pia ujio wa kipaji kipya kwenye komedi, Stan Bakora.
Ni vichekesho vya kwenye redio, ambapo Radio E-FM ndiyo waliowatambulisha. Sioni haya kusema kuwa, wasanii hawa ni kati ya vionjo vilivyoipaisha redio hiyo na kuwa na mashabiki wengi.
Hakuna aliyemjua Stan Bakora kabla ya E-FM, hata Kitale mwenyewe kama asingejiweka wazi mapema, angebaki na umaarufu mara mbili – angekuwa Mkude Simba na wakati huohuo Kitale.
Angeendelea kutesa kwenye filamu za vichekesho kama Kitale, lakini wakati huohuo akitengeneza maisha kwenye vichekesho vya redio na mitandaoni.
Sanaa ya ucheshi siyo kazi ndogo. Isingekuwa rahisi mtu kumpiku au kumfikia Mzee Majuto au Joti kwenye uigizaji wake. Kama Stan Bakora angekuja na staili ya akina Masanja, asingepata mafanikio aliyonayo leo hii.
Unaweza kuona kwamba staili yao ya tofauti ndiyo iliyowabeba na ni kweli kwamba hawafanani na wasanii wengine hapa Bongo kwenye vichekesho vyao.
Achana na Stan Bakora, yupo komediani mwingine anayekwenda kwa jina la Shaphii Omary maarufu JK. Msanii huyu mwenye uwezo wa kuigiza sauti za watu maarufu wakiwemo viongozi, amepata umaarufu zaidi baada ya kuweza kuiga kwa ustadi sauti ya Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete.
Shaphii aliona mbali. Kabla yake, wapo wakali wa kuiga sauti; kuna Steven Nyerere ambaye anapatia zaidi sauti ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, nyuma yake yupo Mc Babu Ayoub, wote hawa ni wakali wa kupatia sauti za watu maarufu.