Yanga yalia kukamiwa
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amesema kutetea ubingwa wao si kazi rahisi kwa kuwa kila timu inayokutana nayo huwakamia kuvunja rekodi yao.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Pluijm alisema kutokana na kutambua hilo, ndio maana wamejiwekea malengo ya kuhakikisha wanapambana kwa kila mchezo kupata pointi tatu.
Alisema kutokana na ubora wa kila timu katika ligi, ni ngumu kuzungumzia mapema kama wataendelea kuwa mabingwa kwa msimu huu, kwani kila timu imejipanga kuonesha uwezo na hamu ya kulitaka taji.
“Laiti kama uwanja ungekuwa unazungumza nani atashinda taji msimu huu, ningetoa nafasi ya kusema, kuna ushindani mkali na kila timu imejipanga dhidi yetu kutuvua ubingwa,”alisema.
Alisema, “lengo letu tunataka kuongoza kwenye ligi ikiwezekana tuje tumalize hivyo, lakini inatubidi tusubiri tuone itakuwaje hadi mwishoni mwa msimu, unajua soka wakati mwingine haitabiriki,”alisema.
Pluijm alisema lolote linaweza kutokea wakati wowote na kila kitu kinawezekana na wakati mwingine huenda kisiwezekane, akiweka msisitizo kuwa anahitaji vitendo vionekane zaidi kuliko maneno.
Yanga inatarajiwa kucheza mchezo ujao dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza wa ligi utakaochezwa nje ya Dar es Salaam.
Ilianza vyema kutetea ubingwa katika mchezo wa kufungua pazia la ligi dhidi ya African Lyon mwishoni mwa wiki iliyopita na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Akizungumzia maendeleo ya wachezaji wake waliokosekana katika baadhi ya mechi zilizopita, akiwemo Obrey Chirwa, Malimi Busungu, Ally Barthez, Juma Abdul na Nadir Haroub waliokuwa majeruhi alisema kuwa tayari wameanza mazoezi mepesi na huenda wakaanza kuonekana katika mechi zijazo.
