“Nimestaafu naomba niachwe nipumzike. Nisingependa kuhusishwa na siasa za mtandaoni dhidi ya Serikali. Namuunga mkono Rais na serikali yake,” ameandika leo Kikwete.
Katika kutilia msisitizo Kikwete amesemema, “Nasikitishwa sana na matumizi mabaya ya picha zangu mtandaoni hususan watu kunilisha maneno kwa kutaka kutimiza malengo yao ya kisiasa.”
JK alisema nini UDSM mpaka kuzua mjadala mitandaoni na katika vyombo vya habari kiujumla?
Rais mstaafu Kikwete ambaye pia ndiye mkuu wa chuo hicho alikuwa akihutubia ndani ya ukumbi wa Nkurumah katika maadhimisho ya miaka 55 ya kuanzishwa kwa UDSM alieleza yafuatayo katika sehemu ya hotuba yake;
“Lazima ukishakuwa mpya watu waone kama kuna mambo mapya, lakini mapya ya maendeleo (akasita na kucheka..), siyo mapya ya kubomoa kule tulipotoka.”
Kauli hii ilitafsiriwa kama ni kuikosoa serikali ya Rais Magufuli kwa namna ambavyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kufumua mfumo wa utendaji uliokuwepo katika awamu iliyopita hata kama baadhi ya mambo hayo ni mazuri.
Baadhi ya mambo yanayotajwa kuwa yalikuwa mazuri lakini Serikali ya Rais Magufuli imeamua kuyabadili ni kurushwa kwa matangazo ya Bunge ya moja kwa moja (live), kutoa uhuru kwa vyombo vya habari na kuruhusu mikutano ya hadhara, kutofukuza wafanyakazi bila kuwapa haki ya kujitetea pamoja na kutoa mikopo ya vyuo vikuu kwa wanafunzi wengi zaidi.