Kwa mara ya kwanza Tanzania imeweza kuweka betri kwenye moyo wa mtoto
Dar es Salaam, Tanzania.Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)-Muhimbili LEO imefanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa mtoto, Happiness John Josephat ambaye amepandikizwa peacemaker (betri ya umeme wa moyo) kwenye mfumo wa moyo wake.
Mmoja wa madaktari wa moyo walioshiriki kwenye upasuaji huo, Dk Godwin Sharau wa taasisi hiyo amesema upasuaji huo umechukua saa moja na kwamba mtoto anaendelea vuzuri.
Dk Sharau amesema mtoto huyo amepandikizwa peacemaker (betri ya umeme wa moyo) ambayo itasaidia kuunganisha mishipa ya fahamu ya umeme wa moyo ambayo inaunganisha vyumba vya moyo vya juu na chini kwenye moyo wa binadamu.
“Upasuaji huu ni wa kwanza kufanyika Tanzania. Upasuaji kama huu unafanyika kwa watu wazima, lakini watu wazima hawahitaji upasuaji wa moyo wa kupandikiza. Watoto wanahitaji upasuaji wa moyo wa kuipandikiza.
“Tatizo la mtoto huyu ni la kuzaliwa. Na ni nadra kutokea. Inaweza kupita miaka mingi bila watoto kutokea tatizo kama hilo. Upasuaji umefanywa kwa ushirikiano wa madaktari wa moyo na madaktari wa matibabu ya moyo nikiwamo mimi (Dk. Godwin Sharau), Dk Michael Valentine kutoka Marekani, Dk Kisenge na Dk Sulende Kubhoja, Dk wa usingizi, Dk Anjelan Muhozya na madaktari wengine ambao wamesaidia katika upasuaji huu,” amesema Dk Godwin Sharau.