Ni uchawi, ushirikina au sayansi ya Kiafrika isiyotakiwa?
MARA nyingi tumesikia viongozi wa serikali wakilaani na pengine kupiga marufuku vitendo vya imani za kishirikina katika jamii kwa madai ya kusababisha chuki, mifarakano na hata mauaji miongoni mwa wanajamii.
Imani hizi ndizo zinazodaiwa kusababisha mauaji ya wanawake vikongwe sehemu nyingi nchini kwa tuhuma za uchawi kwa mtizamo potofu kwamba wachawi siku zote ni wanawake.
Hili ni tatizo la kisaikolojia na kisosholojia ambalo si kusudio la makala haya kulielezea kwa leo; lakini itoshe kutamka tu kwamba kuna ubaguzi na unyanyasaji mkubwa wa kijinsia katika jambo hili; kwamba, wakati neno “mchawi” na “uchawi” (witch/witchcraft) linahusishwa zaidi na mwanamke, mwanaume anayefanya hayo amepewa sifa njema kwa kuitwa “Mganga wa Jadi” (Witchdoctor) au tabibu wa kijadi hivi kwamba jamii haina ugomvi naye kwa sababu ni tabibu.
Kwenye hili, hautapoteza kitu kama utamsoma Mihangwa J; “Violence Against the Aged: Killings on Witchcraft Beliefs in Shinyanga Region”, TAMWA Project; uk. 9, 29).
Serikali kwa upande wake haitambui kuwapo kwa “uchawi” ila inatambua “imani na vitendo vya kishirikina”. Na ingawa Sheria ya Uchawi (Witchcraft Ordinance) ya mwaka 1928, namba 18 (kama ilivyorejewa upya mwaka 2002) inabeba neno “uchawi” (witchcraft), haifafanui wala kutaja “mchawi” ni nani bali kinachotajwa na kufafanuliwa pekee katika kifungu cha pili cha sheria hiyo ni neno “Uchawi” na “kifaa cha Uchawi” (instrument witchcraft) ambapo chini ya kifungu cha tatu na saba, ni kosa la jinai kwa mtu kuwa nacho au kukitumia kwa madhumuni yoyote yale.
Pia kifungu cha nne cha Sheria ya Uchawi, kinatamka kosa la jinai kwa mtu kumwita (au kumtaja) mtu mwingine “mchawi”.
Chini ya Sheria hii, Uchawi umefafanuliwa kujumuisha Ulozi (sorcery); mazingaombwe (enchantment); kuchawia (bewitching); kutumia vifaa vya uchawi na kuwa na au kutumia uwezo wa elimu-fumbo (occult knowledge) inayofahamika kwa watu maalum pekee.
Kifaa cha Uchawi kimetafsiriwa kumaanisha “kitu chochote kinachokusudiwa kutumika au kinachoaminika kuwa na uwezo wa kuzuia au kuchelewesha mtu kutenda au kutekeleza jambo ambalo ni halali kwake kutenda kisheria;
Au kulazimisha mtu kutenda au kutekeleza jambo lililo kinyume na sheria; au kubaini mtu aliye na hatia ya tuhuma ya jinai au kitendo kingine anacholalamikiwa; au kusababisha kifo, majeraha au ugonjwa kwa mtu yeyote au madhara kwa mali; au kumwogofya mtu.
Au kwa kutumia nguvu dunia (supernatural power), kutoa au kuzalisha miujiza kwa njia ya hirizi, kago, talasimu au fingo na dawa zinazofahamika kutumika kwa madhumuni yaliyotajwa hapo juu”.
Mkanganyiko hapa ni kwamba, wakati serikali haiamini uchawi ila imani potofu za kishirikina, Sheria (ya serikali) juu ya uchawi inaendelea kuwapo, kutambua na kufafanua “uchawi” ni nini na adhabu zake.
Umahiri wa sayansi na teknolojia ya kiafrika kabla ya kuingiliwa, kudhibitiwa na hatimaye kuangamizwa na wazungu kwa njia ya ubeberu wa kiroho na kiutamaduni, ulikuwa wa kidunia kabla ya Ulaya haijastaarabika. David Kimble, katika “A Political History of Ghana (1963) anakiri hili akisema:
“Afrika tangu zama za kale ilikuwa ghala na hazina ya Sayansi na Fasihi; kutoka Afrika elimu hiyo ilifundishwa Uyunani (Greece) na Rumi ya kale, kwamba kwa heshima kubwa Wayunani wa kale walimpa Mungu wao kipenzi (mwanamke), Mungu wa Hekima (Wisdom) – Minerva, sura na hadhi ya Kiafrika”.
Waafrika tangu kale waliamini kifo na ufufuo kama ambavyo tu wahafidhina wa dini za mapokeo wanavyoamini. Angalia ushuhuda huu wa Mwafrika kabla ya ubeberu wa kiutamaduni kuvamia kutoka nje, anasema:
“Waliokufa hawako chini ya ardhi: wako kwenye moto unaofifia/wako kwenye majani yanayojililia/wako kwenye miamba na majabali/wako kwenye misitu/wako majumbani/waliokufa hawajafa”.
Tunauliza: Ilitokeaje kwamba wafu wa kigeni wa dini za mapokeo wakaitwa “Watakatifu” wa kupigia magoti na sala, na wa Kiafrika wakaitwa “Mahoka” au “mizimu”, wa kubezwa na kuogopwa?.
Tofauti na mtizamo wa serikali wa kutoamini kuwapo kwa Wachawi na Uchawi, dini za Mapokeo zinatambua kuwapo kwake ambapo “Mchawi” ametafsiriwa kumaanisha mtu yule anayekubali kutumia au kutumika kutenda miujiza kwa nguvu za shetani na kwa kumwasi Mungu (1 Samwel 28:7-14).
Mhimili wa uchawi kwa mtizamo huo ni pepo wachafu (spirits/demons) wanaoweza kutumika kudhuru binadamu na ni pepo wa kizazi cha waovu “Nephilin” (Mathayo 9:34, Daniel 7:10). Wana uwezo wa kurandaranda duniani; mwendo wao ni wa kasi mithili ya mwanga na wanaweza kutumiwa na wachawi kudhuru binadamu na mali (Marko 5:9, 7:26-30; 9:17).
Mwisho, kuna mtizamo huru usio wa kiserikali wala kidini, wa wasomi na wanasayansi wenye kuamini kwamba kile kinachoitwa “Uchawi” kinaweza kuelezeka kwa misingi ya uthibitisho wa kisayansi kwa kuhusisha akili ya kawaida ya mwanadamu.
Wanasema, sehemu kubwa ya kile kinachoitwa “Uchawi”, ni mchezo wa kimazingaombwe kwa “Mchawi” kucheza na akili na uwezo wa kufikiri wa mwanadamu kutoweza kuhimili kisaikolojia.
Wanadai, hata mhubiri wa dini za mapokeo mwenye “karisma” (Charismatic) anaweza kuwafanya wasikilizaji wake wapagawe na kulia ovyo kwa kile kinachoelezwa kuwa “kushukiwa na roho mtakatifu”; lakini inapokuwa kwa dini za jadi, anaitwa mzimu au (kupandisha) pepo mchafu (mashetani) bila wao kujitambua.
Wanakwenda mbali kwa kueleza kuwa, utafiti umeonesha kwamba hata yule “mchawi” wa Kibiblia wa Endori (1 Samweli 28:7-14 hapo juu) hakuwa “mchawi”, na imetafsiriwa kuwa ni “mwanamke aliyekuwa na pepo la kawaida”, kumfanya kifaa cha mawasiliano (medium) cha pepo.
Mtizamo huu pia unadai kuwa, kiethnolojia na kisosholojia, vitu kama runinga, eksirei (X-ray), intaneti na simu, ni sayansi na teknolojia inayostahili kuitwa “vifaa vya uchawi” kama vilivyo tu vifaa vya sayansi na teknolojia ya jadi kwa mujibu wa sheria ya uchawi.
Iko wapi haki na usawa katika kupima na kuhukumu sayansi na teknolojia moja na kusalimisha kwa kukweza nyingine kiholela?, wanahoji.
Mitizamo yote miwili, yaani, mtizamo wa serikali (sheria) kutoitambua sayansi na teknolojia “tata” ya jadi, na mtizamo wa kidini wenye kuibeza sayansi na teknolojia hiyo ni ya kukweza dini, sayansi na teknolojia ya kigeni kwa maangamizi ya sayansi na teknolojia bora ya nyumbani kwa kuinyima uhuru wa kukua kwa sheria mbaya ya uchawi, yenye kuendeleza ukoloni-mamboleo na ubeberu wa kiroho.
Hata hivyo kambi ya fikra huru yenye kuongozwa na utafiti na matokeo ya kisayansi imeshindwa kuwa kiungo bora kwa kusimama njia panda na kutenda kama popo (ndege au mnyama?) katika mtafaruku huu. Je, tuwaiteje hawa: Wakanamungu (atheists) Wayakimfu (materialists) au wadhanifu?
Tunafahamu, dini na utamaduni havitenganishiki kwa kuwa ni msingi mkuu wa uhai na mhimili wa maisha ya jamii. Utamaduni ni pamoja na sayansi na teknolojia inayowezesha jamii kukabiliana na maisha kwa kujitegemea bila msaada kutoka nje.
Dini kwa upande wa pili ni imani katika uwepo wa Mungu (Muumba wa vyote) mwenye nguvu zaidi ya binadamu aliyeumbwa na anayeudhibiti ulimwengu na ambaye pia ni chimbuko na msimamizi mkuu wa utamaduni.
Kwa mantiki hii, hakuna utamaduni wa jamii moja ulio bora kuliko utamaduni wa jamii nyingine, ila tamaduni zinaweza kulishana na kushibishana kwa mambo yenye kushabihiana.
Silaha kubwa kwa Wakoloni wa Kizungu wakati wa kuivamia na kuigawana Afrika, ilikuwa dini ili kuwapumbaza wenyeji wajikane wenyewe kuwa hawakuwa na dini wala Mungu.
Kipindi hiki cha Umisionari, kiliitwa kipindi cha “kutuliza, kustaarabisha na kujenga amani” (Pacification) ili Waafrika wasiinue silaha kupigana na wavamizi. Kipindi kilichofuata baada ya “utulivu” wa kupumbaza kilikuwa ni cha ukoloni wenyewe (Colonization); na pale Waafrika walipojaribu kuzuia kwa njia ya mapambano, walinyukwa kwa silaha za kisasa.
Angalia wimbo huu wa ibada katika moja ya makanisa nchini Nigeria karne ya 19 kuthibitisha hilo: “Onward Christian soldiers, into the heathen lands; Bible in your left hand, rifle in your right one; spread the gospel, with the rattling gun”.
Yaani, “mbele kwa mbele askari wa Kikristo, katika nchi za wasio na dini; Biblia mkono wa kushoto, bunduki mkono wa kulia; ienezeni Injili kwa mtutu wa bunduki itemayo risasi”.
Kuna wazungu wema wanaochukizwa na haya pengine kuliko Waafrika wenyewe, waliokubali utwana na kudhalilishwa kwa utamaduni wa Mwafrika. Padri, Profesa, Dk. Edward Achermann, anaandika kukiri unyama huo, katika kitabu chake, “Cry, Beloved Africa!/Fumbuka Afrika!”, akisema: “Waethnolojisti wote wanakubaliana kwamba Waafrika wamekuwa na hali ya kidini hata kabla ya kufika Wamisionari. Ni kweli kwamba dini yao haikutokana na ufunuo, lakini ilikuwa dini asilia hivi kwamba waliishi kwa umakini mkubwa na kwa ibada ya kweli hata kuzidi wazungu wenyewe”.
Anaendelea, “Waafrika walifuata yale ambayo yamo katika Amri kumi za Mungu…….. waliamini juu ya ufufuo kwamba bado wataishi baada ya kifo kama wanavyoishi mahoka wao “Ahnen”.
Na kuhusu vitu ambavyo sasa vimeitwa “vifaa vya Uchawi”, Ackermann anasema: “Waafrika sio tu walijua maisha ya kimwili, bali pia maisha ya kiroho, dini, elimu adili (yanayoshika ulimwengu wa kiroho na mwili), maadili (yanayounganisha yote mawili pamoja); na ili kuyaishi na kuyafahamu maisha ya kiroho, walitumia shughuli zao za kila siku pamoja na hisia zao kwa njia ya vitu (Tellus mater) wanavyoweza kuvigusa katika ibada na matambiko yao kufanya mambo ya kiroho yaeleweke”.
Nilipata kuulizwa na mwanajadi mmoja swali hili: “Waisraeli waliopelekwa utumwani Babiloni walikataa kuabudu miungu ya nchi hiyo wakihoji kwa kusema: “tutaimbaje wimbo wa Bwana (Mungu wa Israeli) katika nchi ya ugenini?”. Mbona sisi tunapohoji mantiki ya dini za mapokeo, za Mungu asiyejua lugha na utamaduni wetu, tunaitwa wapagani au wachawi?”. Jibu nitalitoa kwenye hitimisho la makala haya.
Mara nyingi tumeambiwa, serikali haina dini ila watu wake wanazo. Kama hivi ndivyo, kwa nini tunaendelea kuwa na sheria inayobana ibada na vifaa vya ibada za dini za jadi kwa sababu tu ya kukweza tu na kuimarisha dini za mapokeo, sayansi, teknolojia na utamaduni wa kigeni pekee?.
Pengine hatuna sababu ya kuendelea kusumbukia hilo kwa sababu Mahakama Kuu ya Tanzania ilikwishatoa msimamo juu ya jambo hili katika kesi ya Thomas Bangili and Samike Maduhu Vs R (1969) HCD 246, kwamba vitendea kazi vya uganga na uganguzi pamoja na shughuli hizo si vya uchawi.
Thomas Bangili na mwenzake waliokuwa waganga wa jadi walipatikana na hatia kwenye Mahakama ya chini kwa makosa matatu chini ya Sheria ya Uchawi (The Witchcraft Ordinance) ya mwaka 1928, ambayo ni (1) kujitangaza au kudai kuwa na uwezo wa Uchawi, (2) kukutwa na kifaa cha uchawi, yaani kibuyu chenye kuongea, na (3) kumiliki na kutoa kwa matumizi haramu chombo cha uchawi (yaani, kibuyu kinachoongea). Walihukumiwa kifungo na baadaye kukata rufaa Mahakama Kuu.
Katika utetezi wake, Thomas Bangili alisema: “Hiki ni kibuyu changu; ninakitumia kuagulia watu. Kibuyu hiki huniambia matatizo yote ya wateja wangu kama vile magonjwa na matakwa yao. Ninatumia mizimu yangu (pepo?) kuelewa matatizo ya wateja, kupitia kibuyu hiki”.
Akiruhusu rufaa yao, Jaji Kimicha (alivyokuwa wakati huo), alibainisha kuwa kwa karne nyingi, jamii zetu zimenufaika na wataalam wa tiba za jadi ambao waliweza kutambua magonjwa ya kawaida na magonjwa tata yanayotokana na uchawi au kulogwa. Waganga hawa hawana maabara, vyumba vya upasuaji wala eksirei.
Kwa kuelewa mapungufu haya, wao hutumia njia ya kupiga ramli, utabiri (divination), tafsiri za ndoto na ishara (omen) na nguvu za mizimu (occult power) maarufu kama fahamu ya sita (sixth sense). Baadhi ya Waganga hao wameweza kutibu na kuponya magonjwa yaliyoshindikana na kujipatia sifa kubwa”, alisema Jaji Kimicha.
Akifafanua neno “Pepo” alisema, lina maana ya viumbe wasioonekana, wanaoweza kumilikiwa na kutumiwa na baadhi ya watu, yaani “wachawi”, kudhuru watu na mali; na kuongeza kuwa, “sheria ya uchawi” haikukusudia kupiga marufuku au kuadhibu wale wanaojishughulisha na ama kubaini au kutibu madhara ya uchawi (spells)”, na kwamba “kubaini au kutibu madhara ya uchawi (na matumizi ya vifaa vyake) si sawa na kujihusisha na uchawi”, na huo si uchawi.
Pamoja na yote hayo, jambo moja ni dhahiri: kwamba Afrika na Mwafrika ameruhusu kirahisi vita vya kiutamaduni kupiganwa kwenye ardhi yake kwa kujijeruhi na kujeruhiwa kwa sababu ya kujikana mwenyewe. Je, haikusemwa kwamba taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mti usiokuwa na mizizi?.