Kumetokea mripuko mkubwa ndani ya kambi ya kijeshi ya Marekani Afghanistan.
Watu wanne wameuwawa Jumamosi (12.11.2016) katika mripuko uliotokea ndani ya kambi kubwa kabisa ya kijeshi ya Marekani nchini Afghanistan na kujeruhi wengine kumi na nne ambapo utaifa wao haukuweza kufahamika mara moja.
Kundi la Taliban limedai kuhusika na mripuko huo uliotokea ndani ya kambi ya kikosi cha anga ya Bagram kaskazini ya mji mji mkuu wa Kabul yenye ulinzi mkali wakati waasi wa kundi hilo wakizidisha mashambulizi yao nchini kote kabla ya kuanza kwa kipindi cha majira ya baridi ambapo kwa kawaida mashambulizi yao hupunguwa.
Msemaji wa gavana wa jimbo la Parwan Waheed Sediqi ambako ndiko ilipo kambi hiyo ya Bagram amesema mripuko huo umesababishwa na mtu aliyejitolea muhanga ambaye amejiripua karibu na eneo la huduma ya chakula ndani ya kambi hiyo.
Sediqi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba bado hawajui utambulisho wa wahanga lakini mshambuliaji ni mmojawapo wa wafanyakazi wa hapo.
Marekani ina takriban wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan ambapo kikosi kikubwa kiko katika kambi hiyo ya Bagram. Shambulio hilo linaonyesha ikiukaji mkubwa wa taratibu za usalama ndani ya mojawapo ya vituo vya kijeshi vyenye ulinzi mkubwa kabisa nchini Afghanistan.
Taliban yadai kuhusika
Kamanda mkuu wa Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Afghanistan John Nicholson ametowa rambi rambi kwa familia na marafiki wa wahanga waliopoteza maisha yao katika shambulio hilo na kuwahakikishia kwamba jamaa zao waliojeruhiwa wanapatiwa huduma nzuri kabisa na wataendelea kuzingatiwa mawazoni.
Msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid amesema kundi hilo la waasi limehusika na shambulio hilo ndani ya kambi ya Bagram na kudai kusababisha maafa makubwa kwa wanajeshi wavamizi wa Marekani.Kambi hiyo ya Bagram imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na waasi wa kundi hilo la Taliban.
Mwezi wa Disemba mwaka jana mshambiliaji wa kujitowa muhanga wa kundi la Taliban aliyekuwa akiendesha piki piki aliuwa wanaheshi sita wa Marekani karibu na kambi hiyo hilo likiwa mojawapo ya shambulio lililosababisha maafa makubwa dhidi ya vikosi vya kigeni nchini humo kwa mwaka 2015.
Kuongezeka mashambulizi
Shambulio hili la Jumamosi linakuja baada ya lori lilosheheni mabomu kubamizwa na ubalozi mdogo wa Ujerumani katika mji wa Mazar-i-Sharif kaskazini mwa Afganistan hapo Alhamisi usiku na kuuwa takriban watu sita na kujeruhi wengine zaidi ya 100.
Kuongezeka kwa mashambulizi hayo dhidi ya vituo vya mataifa ya magharibi kunakuja siku chache tu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa rais wa Marekani uliokuwa na ushindani mkali.
Suala la Afghanistan lilikuwa halikupewa uzito wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Marekani juu ya kwamba hali nchini humo inaweza kuwa suala la dharura kwa rais mpya wa Marekani.
Rais mteule wa Marekani anatarajiwa kurithi vita vya Marekani vilivyochukuwa muda mrefu kabisa na havina dalili ya kumalizika hivi karibuni.