NAKUPONGEZA wewe msomaji mpya wa safu hii. Kama ndiyo unaanza kusoma hapa leo, umechagua sehemu sahihi ya kukuza fikra zako kwenye suala zima la uhusiano, maisha na saikolojia kwa ujumla wake.
Wadau wa kona hii na wale wanaofuatilia kwenye gazeti damu moja na hili, Risasi Mchanganyiko kila Jumatano kwenye safu ya All About Love wanakubaliana na mimi kuwa siku hadi siku maisha yao ya kimapenzi yanakwenda vizuri.
Leo tunajadili eneo muhimu sana katika uhusiano; Uaminifu. Wengi wanaweza kunishangaa kidogo, wakiamini kwamba suala la kuwa mwaminifu linamuhusu mhusika moja kwa moja.
Kwamba kama mtu akitaka kuwa mwaminifu au kinyume chake ni uamuzi wake mwenyewe! Hoja hiyo ni ya kweli, lakini si kwa asilimia zote. Kuna vitu vingine ambavyo vinasaidia kumfanya mtu awe mwaminifu.
Ndugu zangu, wakati mwingine suala la uaminifu si la hiyari! Kuna vitu inabidi vifanyike ili angalau uwe katika wingu la uaminifu, halafu unaongeza na nia yako ya kutaka kuwa mwaminifu, ndipo unafanikiwa.
SAUTI ZA WADAU
Nilipata kuwasiliana na watu wanne wa jinsi tofauti wenye tatizo moja; Wameshindwa kuwa waaminifu. Kutokana na ufinyu wa nafasi, utawasikia wawili kati yao.
Wa kwanza: “Kaka Shaluwa, mimi nina mpenzi wangu ambaye nipo naye kwenye uhusiano, huu mwaka wa tatu. Tunapendana sana. Mimi kama msichana kuna wakati natongozwa na wanaume.
“Kwa sababu ninajua nina mwanaume wangu, huwa nawatosa, lakini wakati mwingine najikuta nakosa nguvu. Nakiri kumsaliti mpenzi wangu mara tatu, ila roho inaniuma sana. Tatizo ni nini kaka yangu? Naomba unisaidie, maana sipendi kumsaliti mpenzi wangu.”
Wa pili: “Mimi ni mwanaume mwenye miaka 37, nimeoa na nina watoto wawili na mke wangu mpenzi. Nimemfuatilia sana, kiukweli ni mwaminifu kupindukia. Hata mimi napenda sana kuwa kama yeye, lakini ndiyo hivyo, nashindwa. Nimeshatoka na wasichana wawili, sipendi kabisa hali hii.”
FUNZO
Kwa maelezo yao, tunaona namna ambavyo watu hao ambao wapo kwenye uhusiano (mwingine kwenye ndoa) lakini wanawasaliti wenzi wao. Hata hivyo, si kwa kupenda – wanafanya hivyo na moyoni wanaumia.
Jiangalie na wewe rafiki yangu mpenzi. Unamheshimu mpenzi/mwanandoa mwenzako kwa kuwa naye peke yake au unamsaliti? Hebu angalia ndani ya nafsi yako, ni jambo unalopenda kulifanya au linakuumiza?
Sikia rafiki yangu, usaliti ni sumu ya mapenzi. Ni mwanzo wa kumkosoa mpenzi wako na kuziona kasoro zake. Habari zaidi ni kwamba, mtu anayechanganya sana wapenzi ni rahisi kupoteza uwezo wa kupenda.
Hujikuta akiwachukia watu wa jinsi ya pili, huongozwa zaidi na tamaa na msisimko wa mapenzi hupungua. Zipo athari nyingine nyingi zinazotajwa kisaikolojia kwa mtu asiye mwaminifu. Wanasaikolojia wanakwenda mbali zaidi – wanasema si ajabu mhusika kuanza kupoteza imani na hata yeye mwenyewe. Hajiamini tena.
UNATAKA KUWA MWAMINIFU?
Huu ndiyo mwongozo wako katika somo hili. Kwa maneno mengine, kama wewe ni msaliti na unapenda tabia yako, ishia hapa. Usiendelee kusoma hii mada maana haikufai. Inawezekana ni mwaminifu na unatamani kuendelea kudumu katika uaminifu wako, ni jambo zuri na mada hii ni kwa ajili yako. Twende tukaone sasa.
WEKA NIA
Si uchawi, ni imani ya ndani ya moyo wako. Kila kitu kinaanza na nia. Kama ni kweli unatamani kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako, anza kujenga hili kuanzia moyoni mwako. Jiambie kuwa unapenda kuwa mwaminifu siku zote na unatamani kuendelea hivyo.
ANZA NA KINYWA
Hili ni jambo la kwanza kabisa kwako wewe ambaye unahitaji kuwa mwaminifu. Nimesema tangu mwanzo kuwa unaweza kuwa na nia ya kutaka kuwa mwaminifu, lakini ukaangushwa na mambo madogo ambayo yatakufanya baadaye ujute.
Kinywa chako ni kitu muhimu sana kuzingatia. Pima maneno yako. Usipende kuzungumza lugha chafu, maneno yasiyofaa au stori za mapenzi (hasa na watu wasio wa jinsia yako).
Inawezekana usione umuhimu wa hili, lakini rafiki yangu, nikuambie kitu kimoja? Unapoweka mazoea ya kuzungumza na marafiki zako mambo ya mapenzi, ni rahisi sana kujiingiza kwenye usaliti.
Utaanza kama burudani, mipaka ikishavukwa utajiona sehemu ya stori zenu. Namaanisha unaweza ukatamani au kuvaa uhusika wa stori yenyewe, hapo sasa inakuwa rahisi kuingilika hata kama nia yako haikuwa hiyo.
Zungumza kwa busara, achana na utani usio na maana. Kinywa chako kioneshe namna unavyojiheshimu. Kama una mazoea ya kujenga utani sana, ni rahisi mtu kukujaribu kimapenzi, akiwa na ngao ya utani!
Ukikubali amekubeba, ukikataa anakuambia: “Nilikuwa nakutani bwana...hutaniwi wewe?”
Umeona eeh?!
Basi sawa...ngoja nipumzike hapa kwa leo. Endelea kuyatafakari haya, wakati ukisubiri wiki ijayo kwa mwendelezo wake.