Jaji Kaijage anachukua nafasi ya Jaji (mstaafu), Damian Lubuva, ambaye anaondoka katika ofisi hiyo kuu ya usimamizi wa uchaguzi nchini akiwa ameacha viporo kadhaa vya kazi. Viporo hivyo ni pamoja na ukamilishaji wa mchakato wa katiba mpya.
Katika mchakato huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inapaswa kusimamia upigaji wa kura ya maoni ili wananchi wapate fursa ya kuipitisha au kuikataa rasimu ya Katiba Mpya iliyojadiliwa, kufanyiwa marekebisho na hatimaye kupitishwa na lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK).
Mwenyekiti huyo mpya anayechukua nafasi ya Lubuva ambaye muda wake wa kukaa ofisini umekwisha rasmi kisheria Desemba 19, mwaka huu, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ataongoza tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Jaji (mstaafu) Hamid Mahamoud Hamid kuendelea na wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa NEC baada ya muda wake katika wadhifa huo kukamilika Desemba 19, mwaka huu, kama ilivyokuwa kwa Jaji Lubuva.
Rais Magufuli pia amemteua Jaji (mstaafu) wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Harold Reginald Nsekela kuwa Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Desemba 20, 2016, akichukua nafasi ya Jaji (mstaafu) Salome Kaganda ambaye amestaafu tangu Desemba 10, mwaka huu.
Mbali na teuzi hizo, Rais Magufuli vile vile amewateua majaji wanne wa Mahakama Kuu kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia leo, Desemba 22, 2016.
Waliteuliwa ni Jaji Dk. Gerald Ndika, Jaji Jackobs Mwambegele, Jaji Rehema Kiwanga Mkuye na Jaji Sivangilwe Mwangesi. Wateule hao wote wataapishwa siku inayofuata baada ya uteuzi huu kutangaza rasmi, yaani Desemba 22, 2016, saa tatu asubuhi Ikulu Dar es Salaam.