Kali ya Mwaka : Nyoka wa Maajabu azua Taharuki Afa na Mtu Wake, RUVUMA
Nyoka anayedaiwa kuhusika kwenye Tukio |
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma jana walikumbwa na taharuki baada ya Denis Komba ( 26 ) mkazi wa eneo la Mateka katika manispaa hiyo kufariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa alikuwa amekodi pikipiki kutoka kijiji cha Mpitimbi kilichopo wilaya ya Songea huku akiwa amembeba Nyoka aliyekuwa amehifadhi kwenye mfuko wa koti lake alilokuwa amelivaa na kisha nyoka huyo kuwawa na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji alisema kuwa tukio hilo limetokea Desemba 26 mwaka huu majira ya saa 1.30 usiku huko katika eneo la barabara karibu na ofisi za kampuni ya simu Tanzania ( TTCL ) iliyopo Songea mjini jirani na Hospital ya serikali mkoa huo.
Mwombeji alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio mwendesha Bodaboda yenye namba za usajili MC 724 AKB aina ya SUNLG ,Kasiani Haule ( 24 ) mkazi wa kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea alikuwa amekodiwa na Komba kutoka Mpitimbi kuelekea Makambi manispaa ya Songea ambapo walipofika kwenye eneo la kampuni ya simu mwendesha pikipiki ghafla alishistuka baada ya kuona kunakitu kinamtekenya mgongoni na alipogeuka nyuma kumuangalia abiria wake ghafla aliona kichwa cha nyoka kikiwa kinamgusa eneo la mabegani mwake.
Alisema kuwa inadaiwa kuwa baada ya kumuona nyoka yupo mgongoni kwake alishituka na kuanza kuyumba huku abiria Komba akimsii asipige asiogope na wala asipige kelele ya aina yoyote jambo ambalo mwendesha bodaboda huyo ashindwe kuvumilia na hatimaye aliruka kwa kuiacha pikipiki ikiwa na abiria wake nyuma.
Alifafanua kuwa idaiwa Haule alipiga kelele za kuomba msaada ndipo watu walijitokeza kumpa msaada na walipofika waliona Komba akijaribu kumkamata nyoka ambaye alikuwa amemhifadhi kwenye koti lake alilokuwa amelivaa ambapo baadaye nyoka huyo aliruka kwenye mfuko wa koti na kuanza kukimbia wakati huo wananchi walikuwa wameshafika katika eneo la tukio na kuanza kupambana na nyoka huyo ambaye alikimbilia kwenye karavati huku Komba akiwaomba wasimuue.
Alisema kuwa nyoka huyo akiwa kwenye karavati wananchi walimpiga mawe hadi walifanikiwa kumuua na kwamba baada ya nyoka huyo kuuwawa inadaiwa Komba alianza kutokwa na povu mdomoni mithiri kama ya mtu aliyekunywa sumu ambapo baadae jeshi la polisi liliwachukua wote wawili mwendesha bodaboda na abiria wake kuwapeleka Hospital ya serikali ya mkoa wa Ruvuma ambapo Komba alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospital na mwendesha bodaboda alipatiwa matibabu na kuruhusiwa.
Kamanda alieleza kuwa Nyoka huyo anayekadiliwa kuwa na urefu wa futi tano na sita baada ya kuuwawa alikabidhiwa kwenye ofisi za idara ya Maliasili kwa lengo la kwenda kumfanyia uchunguzi zaidi ili kujua ni Nyoka wa aina gani.
Kamanda Mwombeji alieleza kuwa mwendesha bodaboda Haule baadae ilibainika kuwa alikuwa anaendesha pikipiki hiyo bila kuwa na Leseni na kuwa jeshi la polisi linaendelea kumhoji ili kuona namna ya kumfikisha mahakamani kujibu shistaka linalomkabili.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospital ya serikali ya mkoa Songea Dr, Magafu Majura alithibitisha kuwa Desema 26 mwaka huu aliwapokea watu wawili ,Denis Komba na Kasiani Haule ambapo Denis Komba alifariki dunia kabla hajaanza kupatiwa matibabu na kwamba kwa hivi sasa mwili wa marehemu Komba unafanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo chake japo kuwa mwili huo hauna majeraha yeyeyote.