Namna Magufuli alivyopimana ubavu na akina Kagame Ikulu

Rais John Magufuli na Rais Paul Kagame wakisalimiana hivi karibuni
Viongozi hao wa nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania na Kenya, walikutana Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya jumuiya hiyo ikiwamo mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi (EPA) ambayo nchi za EAC zinataka kuingia na zile za Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Habari za kuaminika ambazo gazeti hili limezipata kutoka katika vyanzo vyake vya kuaminika zinaeleza kuwa Rais Magufuli ndiye aliyekiongoza kikao hicho cha viongozi kwa wadhifa wake kama Mwenyekiti wa sasa wa EAC.
Mmoja wa mashuhuda wa mkutano huo ambaye hata hivyo gazeti hili halitamtaja jina lake kwa sasa, alieleza kuwa Magufuli alikuwa na wakati mgumu kwa sababu nchi za Kenya, Rwanda na Uganda zilikuwa zimejiandaa kufanikisha kusainiwa kwa mkataba huo wa EPA.
Katika mkutano huo, Rwanda iliwakilishwa na Rais Paul Kagame huku Uganda ikiwakilishwa na Rais Yoweri Museveni na Kenya ikiwakilishwa na Makamu wa Rais, William Ruto.
“ Ruto, Kagame na Museveni walikuja kwenye mkutano ule wakiwa wamejiandaa. Kuna uwezekano kuwa walizungumza kabla ya kuja Dar es Salaam. Burundi walisema wao wamewekewa vikwazo vya kiuchumi na EU na hivyo hawawezi kuingia mkataba wowote kwa sasa.
“ Magufuli kwa kweli alifanya kazi kubwa. Alitumia muda mrefu kuwaeleza wenzake sababu za kwanini Tanzania haitaki kusaini mikataba hiyo na nchi za EU. Alieleza athari za mkataba huo kwa viwanda vya Tanzania na nchi za EU kwa ujumla.
“ Magufuli alitumia muda na Uenyekiti wake vizuri. Kwa mfano, alitumia suala la Burundi kutaka muda wa majadiliano na EU kuhusu EPA uongezwe kwa miezi mitatu. Hili la kuongezewa muda ni la Magufuli na si mwingine yeyote,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kingine cha gazeti hili kimeeleza kwamba kwenye suala la Burundi, Magufuli alipendekeza kuwa kwa kuwa mkataba wa EPA unazungumzia nchi zote wanachama wa EAC, ni vema wakasubiri pia kutulia kwa hali ya nchi hiyo ili nayo iingie kwenye mikataba hiyo.
“ Nimeambiwa kwamba kwenye mkutano ule, Magufuli aliwahoji viongozi wenzake kuwa EU waliamua kuiwekea vikwazo Burundi bila ya kuwashirikisha wanachama wengine wa EAC. Kutokana na hilo, aliomba nchi hizo zionyeshe solidarity (umoja) na Burundi kwa kutaka nayo iwe sehemu ya makubaliano hayo,” gazeti hili limeambiwa na mmoja wa wana diplomasia wa Kenya walio karibu na serikali ya nchi yao.
Gazeti hili linafahamu kwamba Ruto, aliyehudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, aliuambia mkutano huo kwamba ni muhimu kwa nchi za EAC kusaini mkataba huo kwa vile nchi yake itaathirika sana endapo hautasainiwa.
Inafahamika kwamba mkataba wa EPA una manufaa makubwa kwa sekta ya kilimo cha maua ya Kenya; ingawa wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaona kwamba wanaofaidika ni matajiri wakubwa pekee na si masikini wa chini.
Raia Mwema limeambiwa kwamba Museveni, Kagame na Ruto walikuja na hoja kwamba endapo hawatasaini EPA, watakuwa wameiumiza Kenya ambayo imeajiri maelfu ya watu kwenye eneo hilo na mwakani inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu ambapo masuala ya uchumi na ajira yatakuwa kipaumbele.
“ Akina Museveni walikuja na hoja kwamba viongozi wa nchi za EAC wanatakiwa kuwaunga mkono wenzao wa Kenya katika kipindi hiki. Hoja ni kwamba nchi hiyo itakuwa na uchaguzi wake mkuu mapema mwakani na kama sekta ya maua itatikisika, kuna uwezekano wa watu wengi kupoteza ajira.
“ Sasa kama watu watapoteza ajira zao, itakuwa ni ngumu sana kwa serikali ya Kenyatta kushinda uchaguzi. Kwa sababu hiyo, ndipo akina Museveni wakaja na hoja kwamba viongozi wanatakiwa kuwasaidia wenzao wa Kenya,” taarifa kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa mkataba huo utaharibu azma yake ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda; kwani mkataba unataka bidhaa zinazotoka Ulaya zipunguziwe ushuru kwa kiasi cha asilimia 90 wakati zinapoingia katika nchi za EAC.
Kuna kipindi, Raia Mwema linafahamu, wakati wa mkutano huo wa marais, Rais Magufuli alijieleza kwa kipindi kirefu kiasi kwamba ilibidi Kagame alalamike; “ “Mwenyekiti, umezungumza kwa kipindi kirefu, naomba uachie na wengine wazungumze”.
Ingawa Magufuli amewakuta wenzake hao madarakani, gazeti hili limeelezwa kwamba kilichofanya hoja za Tanzania zipitishwe ni namna rais huyo alivyoamua kuonyesha hatakubali jambo ambalo halina maslahi kwa nchi yake.
Gazeti hili lina taarifa kwamba ingawa nchi hizo kimsingi zimekubaliana kusubiri hadi Januari mwakani, kuna uwezekano Kenya na Rwanda zikaendelea kivyao na mikataba hiyo ya EPA pasipo kusubiri.
Mmoja wa wanadiplomasia wa Kenya waliozungumza na gazeti hili baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa viongozi alisema wanaweza wasisubiri kwa sababu “hawana imani kama Tanzania itasaini mkataba huo hata baada ya miezi hiyo mitatu.”
Kwa nini EPA ni mbaya kwa Tanzania?
Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, mkataba huo wa EPA utasababisha Tanzania kupoteza mapato ya ushuru wa forodha yenye thamani ya dola milioni 865 katika kipindi cha miaka 25 ya utekelezaji wa mkataba. Akiandika katika ukurasa wake binafsi wa facebook mwishoni mwa wiki iliyopita, Zitto alisema hasara hiyo itatokana na sababu mbalimbali kama vile; Hasara hii itatokana na sababu zifuatazo; “Kwa ushuru kwa bidhaa kutoka EU. Tanzania itaondoa vikwazo vya ushuru kwa asilimia 90 kwa bidhaa zote za kutoka EU ambazo si za kilimo na asilimia 10 kwa bidhaa za kilimo kutoka EU “Hii maana yake ni kwamba Tanzania itaendelea kuwa muuzaji wa malighafi na mnunuzi wa bidhaa zilizoongezwa thamani. Kuondolewa Kwa vikwazo vya ushuru kwa bidhaa za kutoka EU kutapelekea ' trade diversion ' yaani mchepuko wa biashara kwani bidhaa za EU zitaondoa bidhaa kutoka nchi nyingine na hivyo kuondoa mapato ambayo Tanzania ingepata kutoka bidhaa hizo kutoka nchi nyingine. “Kwa kutumia takwimu za Eurostat na kulinganisha na takwimu za ITC Trade Map na nyongeza ya ' Market Access ' ya EAC mtaalamu Jacques Berthelot ameonyesha kuwa Afrika Mashariki nzima itapoteza jumla ya Euro bilioni 3.6 (zaidi ya shilingi trilioni 8) mpaka mwisho wa miaka 25 ya utekelezaji wa mkataba huo. “Mkataba wenyewe wa EPA unatambua hasara hii. Ibara ya 99.1 ya mkataba inasema " wabia wa mkataba huu wanatambua kuwa kuondolewa kwa ushuru kama ilivyo kwenye mkataba ni changamoto kwa nchi za EAC. Wabia wa mkataba wanakubali changamoto hii mahususi lazima ipatiwe majawabu kwa kuweka Mfumo wa fidia". “Hata hivyo EU haijaweka hata sentensi moja ndani ya mkataba inayoonyesha namna fidia hiyo itafikiwa na kulipwa kwa nchi za EAC. Jumuiya ya Ulaya inapendekeza kuwa nchi za EAC zipandishe kodi ya VAT ili kufidia mapato yatakayopotea. “Madhara ya hili ni umasikini mkubwa wa watu wetu kwani bei za bidhaa zitapanda maradufu. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linasema " Nchi masikini zikipunguza mapato yake ya ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zinaweza kufidia kwa njia nyingine kwa asilimia 30 tu. “Ibara ya 14.2 ya mkataba inakataza Tanzania kuweka kodi kwenye mauzo nje ( export taxes ) bila ya ruhusa ya EU. Leo hii Ethiopia inaanza kuuza viatu nje kwa sababu iliweka zuio la kuuza ngozi nje na hivyo kuzalisha ajira ndani ya nchi yao. Historia ya dunia inatuonyesha kuwa hakuna Nchi yeyote duniani ambayo iliendeleza viwanda bila kuvilinda vikue. “Tanzania ijenge uwezo wa ndani kwanza kabla ya kuingia kwenye mikataba ya kuendeleza ukoloni mamboleo. Masharti ya WTO yanatupa nafasi ya kuendelea kuuza Kwa Soko la EU bila kodi. Hakuna haja ya kufungua Soko letu Kwa Nchi za Ulaya katika masharti haya ya sasa. Hili sio suala la itikadi; kwamba tunaopinga Ni watu wa Mrengo wa kushoto. Hili Ni suala la kulinda Nchi yetu na kukataa kutawaliwa kiuchumi,” aliandika Zitto. |
