Jeuri ya walimu:Huna Sh. 200 ya uji bakora
Uji huo unadaiwa kuwa unauzwa shuleni hapo na walimu wanaoshirikiana na mkazi mmoja anayeishi eneo la Goba na kila inapofika saa nne asubuhi wanafunzi wote hutakiwa kupanga mstari kwa ajili ya kwenda kuununua na wasiokuwa na fedha huchapwa viboko na kurudishwa nyumbani.
NIPASHE limezungumza na baadhi ya wanafunzi waliofukuzwa shuleni kwa kukosa Sh. 200 za uji na kuthibitisha walimu kuwachapa na kuwafukuza.Wanafunzi hao majina (tunayo), walidai kuwa imekuwa kawaida kila siku kulazimishwa kununua uji kila inapofika saa nne asubuhi wakati wa mapumziko.
Licha ya kuchapwa viboko, wanafunzi hao pia walidai kwamba baadhi ya walimu wanawalazimisha wawakague kama wamekula kitu kingine kwa fedha ambazo wangetakiwa kununulia uji huo.
“Walimu wanatuambia tufungue midomo ili watukague kama tumekula sambusa, karanga, ubuyu, mihogo ama kitu kingine,” alisema mmoja wa mwanafunzi wa shule hiyo anayesoma darasa la nne.Baadhi ya wazazi waliozungumza na NIPASHE walithibitisha watoto wao kuwaomba Sh. 200 kila siku kwa ajili ya kununulia uji.
Wazazi hao wanapinga utaratibu unaotumiwa na walimu hao na kusema kuwa mwalimu hatakiwi kujihusisha na biashara ya namna hiyo badala yake anatakiwa atumie muda wake kufanya kazi ya kufundisha.Wanasema siyo kila mtoto anapenda kunywa uji wa mchele na kwamba ni kinyume cha utaratibu kumwadhibu mwanafunzi na kumfukuza shule kwa kushindwa kununua uji.
Wakizungumza na NIPASHE kwa sharti la kutotaja majina yao kwa kuhofia watoto wao kuendelea kuandamwa na walimu, wazazi hao walisema licha ya kudaiwa Sh. 200, lakini pia kumekuwapo na michango mingi ambayo inaanzishwa na walimu bila wazazi na walezi kujulishwa rasmi na uongozi wa shule.
Baadhi ya michango waliyotakiwa kuchangia ni Sh. 55,000 kwa ajili ya kugharamia watoto wao kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyoko mkoani Morogoro.Baadhi ya walimu waliotajwa kuhusika kuwafukuza watoto shule walipotafutwa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi, walikataa kuzungumza huku wakidai kwamba hakuna mwanafunzi aliyefukuzwa.
Hata hivyo, Mkuu wa shule hiyo, Sylivester Mbandwe, alithibitisha kuwapo kwa mradi huo unaoendeshwa na walimu na mtu anayepika uji huo, lakini alisema hakuna mwanafunzi aliyechapwa viboko wala kufukuzwa kwa kukosa Sh. 200 ya uji.Makamu Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Solomon Ruta, alithibitisha kupokea malalamiko ya wanafunzi kufukuzwa kwa kushindwa kununua uji.
Ruta alisema wazazi walikubaliana watoto wao kupikiwa uji shuleni hapo na kuuziwa kwa Sh. 200 kwa hiari, lakini hawakukubaliana wale wasiokuwa na fedha wafukuzwe.Aliongeza kuwa walimu wamekuwa wakijiamuria mambo na kupuuza kamati ya shule ambayo ilichaguliwa na wazazi wa wanafunzi.
Alisema walimu hao wamekuwa wakianzisha michango bila idhini ya kamati ya shule ambayo ndiyo inayosimamia shule na kutoa mfano kuwa wamekuwa wakituma barua kwenda kwa wazazi na kuwaomba fedha.
“Mimi nimechoka na walimu wale, wanajiona wapo juu ya sheria, wamegeuza shule kama mali yao, wanatumia mali mbalimbali za shule kama mali zao binafsi na tukisema wanakuwa wakali,” alisema Ruta.
Alifafanua kuwa kamati yake ilitarajiwa kukutana jana kujadili matatizo yaliyopo shuleni hapo na Jumamosi ataitisha kikao cha wazazi wote ili wapewe taarifa.Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema hakuna mwalimu mwenye mamlaka ya kumfukuza mwanafunzi anayekosa fedha za kununulia uji.
Alithibitisha kwamba serikali inatambua utaratibu wa wanafunzi kunywa uji, ama kula chakula cha mchana wanapokuwa shuleni, lakini alisema suala hilo ni la hiari na hakuna mtu anayelazimishwa.
Mulugo alisema mtoto hapaswi kupewa adhabu ya viboko pamoja na kurudishwa nyumbani kwa kukosa fedha za kununulia chakula ama uji.Wanafunzi katika shule kadhaa nchini wamekuwa wakinufaika kwa uji na chakula cha mchana ukiwa ni msaada kutoka Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupitia utaratibu wa wazazi kuchangia.