Papa Francis ataka watoto walindwe
Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amewataka Wakristo kuwakumbuka watoto walio na mazingira magumu wakati wa msimu huu wa Krismasi, huku ulinzi ukiimarishwa kwa hofu ya mashambulizi ya kigaidi mwahala mwingi.
Akiwahutubia maelfu ya waumini waliokusanyika kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Rome katika Mkesha wa Krismasi, kiongozi huyo wa kanisa lenye waumini bilioni 1.2 ulimwenguni alisema Wakristo hawapaswi tu kumfikiria Mtoto Yesu akiwa kwenye kikapu, lakini pia "watoto waliojificha kwenye mahandaki wakikimbia mabomu, wale waliolala nje kwenye miji mikubwa na waliozama chini kwenye maboti yanayosheheni wahamiaji."
"Yesu alizaliwa huku akikataliwa na baadhi ya watu na kuchukuliwa na wengi wengine kama kiumbe tafauti," alisema Papa Francis, akiongeza kwamba hisia hizo za utafauti zinaonekana hadi leo, pale ambapo Krismasi imegeuka kuwa karamu za kulishana wenyewe kwa wenyewe, taa zinapowashwa kwa biashara na "tunapojali zaidi zawadi lakini tukiwa na nyoyo ngumu kwa wale waliotengwa."
Mtawa huyo kutoka Argentina, mara kadhaa hutumia sherehe kubwa kama hizi kuzungumzia masuala ya amani, mabadiliko ya tabia nchi na wahamiaji, na wakosoaji wake wamembandika jina la "mfuasi wa Marx" kwa sababu ya kuukosoa mfumo wa kiuchumi wa kibepari, akitoa wito wa kuwepo usawa kwenye ugawanyaji wa rasilimali za dunia.
Kupotea kwa matumaini na imani
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani alitumia hotuba yake ya Krismasi kwa taifa kutoa wito wa kujikinga na chuki dhidi ya wahamiaji na mpasuko wa kijamii, licha ya mashambulizi ya Berlin.
Mjini Bethlehem, Palestina, ambako inaaminika ndiko alikozaliwa Yesu miaka 2016 iliyopita, waumini walikusanyika hali kukitandwa na habari za uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuilaani Israel kwa utanuzi wa makaazi ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi.
Askofu Pierbattista Pizzaballa anayeongoza Kanisa Katoliki mjini Bethlehem alisema watu wote wamekuwa wahanga wa hisia za ukosefu wa usalama na kutoaminiana.
"Matumaini ya amani hufadhaishwa mara kwa mara, ghasia kwenye mashambulizi ya mara kwa mara, hotuba nyingi za balagha hutufanya turudi nyuma, tufunge milango, tuweke mifumo ya uchunguzi, tukimbie mbali badala ya kubakia kupambana kwa imani na matumaini." Askofu Pizzaballa ambaye amechukuwa nafasi ya Askofu Fouad Twal, aliyefikia muda wa kustaafu, alikosoa tabia ya kufunga milango na mipaka ya mataifa kwa wale wanaoomba hifadhi.
Ghasia na mauaji dhidi ya jamii za Kikristo katika mataifa ya Syria, Iraq, Misri na Jordan zilitajwa kuwa zinaendelea hadi wakati huu, miaka 2016 tangu kuzaliwa kwa kiongozi wa dini hiyo.
Sherehe za mwaka huu zinafanyika katika wakati ambapo wasiwasi umetanda barani Ulaya, baada ya raia wa Tunisia, Anis Amri, kulishambulia Soko la Krismasi jijini Berlin na kuuwa watu 12 na kuwajeruhi wengine wapatao 50. Baadaye, mshambuliaji huyo aliuawa mjini Milan, Italia, siku nne baada ya kukimbia.
Nchini Ujerumani kwenyewe, Rais Joachim Gauck aliitumia hotuba yake ya Krismasi kuwataka Wajerumani kujiepusha na kutawaliwa na hisia za chuki na woga dhidi ya wageni, licha ya mashambulizi hayo ya Berlin.
"Hususani katika wakati wa mashambulizi ya kigaidi, hatupaswi kuongeza kina cha mipasuko katika jamii yetu, ama kuyashuku makundi ya wengine ama kuelekeza vidole kwa wanasiasa,"