UVCCM WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI KWA KUWACHUKULIA HATUA MAOFISA WAKE KAGERA
Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali kuwasimamaisha kazi, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani maofisa watano wanaotuhumiwa kufungua akaunti bandia kwa lengo la kuiba fedha za michango ya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.Umoja huo umesema mashirika mengi ya umma, taasisi za serikali, viwanda na kampuni zilizoanzishwa wakati werikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kujenga uchumi na kutanua wigo wa ajira vilikufa kwa uzembe.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kaimu katibu huyo mkuu alisema ili nidhamu ya uwajibikaji serikalini iweze kuzingatiwa haukana namna nyingine zaidi ya kuwawajibisha wanaokiuka utaratibu na kutengeneza njama za kula fedha zinazotengwa kwa ajili ama ya maendeleo au kusaidia wenye shida kama waathirika wa tetemeko hilo.
Alisema UVCCM inampongeza Rais Dk. John Magufuli na serikali yake na kuitia shime isirudi nyuma badala yake itimiza majukumu na wajibu wa kikatiba na kisheria bila kumfumbia macho mtumishi, kiongozi au hata mzee ambaye huko nyuma alishiriki kwenye ufisadi au uovu.
“UVCCM inavipongeza vyombo vya dola kuwafikisha mahakamani aliyekuwa Ofisa Tawala Mkoa (RAS) wa Kagera, Amantius Msole, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Kelvin Makonda, aliyekuwa Mhasibu wa Mkoa Kagera Simbaufoo Swai na Meneja wa CRDB Kagera, Karlo Sendwa,”alisema.
Shaka alisema kwa kuwa watuhumiwa hao wako mahakamani, UVCCM inaamini utaratibu wa kisheria utachukua mkondo wake. Mahakama ni eneo la utoaji haki, anayetuhumiwa kwa kesi huweza kuingizwa hatiani kwa mujibu wa sheria, kuachiwa huru au kuhukumumiwa bila shinikizo lolote.
“Utendaji wa serikali katika dhamira ya kukuza dhana ya uwajibikaji, uadilifu, uzalendo na uwazi, usibaki serikalini pekee, UVCCM tunaahidi kila panapo na uchafu ndani ya jumuia kama wizi, ubadhirifu au ukwapuaji wa mali tutapekuwa, watakaobainika watachukuliwa hatua,”alisema.
Shaka alisema juhudi za serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere zilipotea kutokana na waliokabidhiwa dhamana kutotimiza wajibu na kusababisha kampuni, viwanda na mashirika ya umma kufilisika na kufa kabisa jambo alilosema halipaswi kujirudia kwenye awamu hii ya sasa.
Alisema serikali ya Mwalimu Nyerere ilianzisha kampuni za umma ikiwemo Aisco, Gapesco, BET, Kioo, Nedco, Bhesco, Napoco, Narco, Dafco, Dapco, Tacoshil na Nasaco ambazo zote zimekufa na waliozisababishia kufa wakiendelea kula maisha mjini bila ya kuchukuliwa hatu.
“Badala yake tukashuhudia walioongoza aidha taasisi, kampuni , viwanda na mashirika ya umma wakitamba na kujenga makasiri ya kifahari, kumiliki magari na miradi isiyolingana na vipato vyao halali,”alisema Shaka.
Alisema serikali ilifanikiwa kuanzisha na kuvisimamia viwanda mbalimbali kikiwemo Urafiki, Sungura Textile, Mutex, Ufi, Kizaku, viwanda vya kabungua korosho Dar es salaam, Mtwara na Pwani, Fishnet, Mtibwa Sugar na Kilombero ambavyo vilizalisha bidhaa tofauti kama Super Ghee, Pride, sabuni za Kodrai na Mbuni na Garnenia, mafuta ya kula yatokanayo na karanga, alizeti na Pamba.
Shaka alisema mashirika kama Shirika la Mabasi ya Taifa (KAMATA) na Usafiri Dar es Salam (UDA) ambayo hivi sasa ama hayapo au ufanisi wake ni duni kampuni za uchukuzi mikoani kama Kauru, Moretco, Kauma, Shirika la Reli yaliweza kumiliki mali mbalimbali ambazo kwa sasa hazipo.
“Yako wapi yote haya, tulikuwa na Shirika la Usafirishaji Mikoani (UMITA), kiwanda cha viatu Bora, viwanda vya ngozi na beteri National. Vyote sasa havipo, tujiulize vilikwenda wapi, vilisibiwa na nini, kina nani walivihujumu, je walifikishwa mahakamani?”alihoji Shaka.
Alisema UVCCM inaunga mkono kinachofanywa sasa na serikali ya awamu ya tano kwa kuwa itafanikisha mkakati wa taifa kuwa la viwanda kwa kuwa aina ya viongozi wadokozi na walafi ndio waliolirudisha nyuma taifa.
Aidha, Shaka alimuomba Rais Magufuli kutowaonea haya baadhi ya wanasiasa wakongwe wakiwemo waliowahi kushika nafasi nyeti na kusababisha madhara mbalimbali lakini sasa wamekuwa wakijitokeza hadharani na kupinga juhudi zake za kudhibiti uhujumu kama uliowahi kutokea.
“Hawa wazee ni matata kwani badala ya kuwatia moyo viongozi wachapakazi na wazalendo wamekuwa wakiwavunja moyo. waache upekepeke na kutomuunga mkono Rais Dk Magufulikama yaliwashinda waliokuwa kwenye nyadhifa basi wasiwe sababu ya kulazimisha kutolewa kwa nafasi ili yaendelee kufanyika hivi sasa” alisema.