Uchumi wayumba, benki zawabana zaidi wakopaji
WAFANYABIASHARA wa sekta mbalimbali za uchumi nchini wanaendelea kukumbwa na hali ya ukata kutokana na taasisi za kibenki kupunguza kwa kiwango kikubwa utoaji wa mikopo.
Hali inayotafsiriwa kuwa huenda ikaathiri ukuaji wa uchumi, inatajwa kuweza kusababisha kushindwa kupanuka kwa shughuli za uwekezaji nchini, hasa kwa wale wanaotegemea fedha zinazotokana na vyanzo vya ndani vya mikopo.
Pamoja na kushuka kwa kasi ya utoaji wa mikopo, hali ya kifedha kwenye sekta ya benki inadaiwa kuimarika kwani riba ya mikopo baina ya benki imeshuka hadi kufikia kiwango cha asilimia 15, kiwango kidogo katika kipindi cha miezi minne mfululizo.
Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi tayari imekuwa bayana kwani ripoti ya muhtasari wa uchumi kwa robo ya pili ya mwaka iliyoishia mwezi Juni mwaka huu imeonyesha kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi ilipungua hadi asilimia 5.5 kutoka asilimia 5.7 kwa robo ya kwanza ya mwaka.
Inatarajiwa kuwa, kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, huenda pia kukaonekana kwenye robo ya mwisho ya mwaka huu, inayoishia Desemba, kwani viashiria vya uchumi havionekani kuleta matumaini.
Ukuaji wa uchumi unachochewa hasa na sekta za kilimo, biashara, utawala, fedha, bima, usafiri na viwanda, lakini sekta hizo zimeendelea kupata huduma hafifu ya mikopo kutoka kwenye sekta za fedha nchini.
Kwa mujibu wa ripoti ya mapitio ya uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwezi Septemba, ukuaji wa sekta ya mikopo umeshuka kutoka asilimia 24.1 mwezi Agosti mwaka jana hadi asilimia 13.8 mwaka huu, takribani asilimia 45.
Sekta zilizokumbwa na hali hii ni kilimo, ambacho ukuaji wa mikopo umeshuka hadi kufikia asilimia 1.4 mwezi Agosti mwaka huu, kutoka asilimia 12.9 mwezi Agosti mwaka jana na sekta ya viwanda kutoka asilimia 36.7 mwezi Agosti mwaka jana hadi asilimia -13.3 kwa mwezi Agosti mwaka huu.
Ripoti hiyo imebainisha kwamba hali hii inatokana na kusita kuendelea kutoa mikopo kutoka benki za biashara, hasa kipindi hiki ambacho inadaiwa kwamba “wanajiweka sawa kuendana na sera mpya za uchumi” za serikali ya awamu ya tano.
Profesa Honest Ngowi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Mzumbe anasema kinachoonekana sasa ni hali ya kawaida kiuchumi hasa pale serikali zinapobadilika (madarakani).
“Kwa kuwa tuna serikali mpya, wawekezaji wengi wanatumia kitu kinaitwa ‘wait and see’ yaani tusibiri ‘tuone kabla’ ya kufanya maamuzi ya kuwekeza ama la,” alisema kwenye mazungumzo ya simu na Raia Mwema.
Profesa Ngowi anasema, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kupambana na ukwepaji kodi pamoja na makusanyo ya malimbikizo ya kodi kwa wafanyabiashara.
“Naweza kusema kwamba baada ya hatua hizi, huenda wafanyabiashara wengi waliamua kukopa fedha zaidi kulipa madeni na hii imesababisha wengi wao kupungukiwa uwezo wao wa kukopa,” alisema.
Pia, suala la kubana matumizi kwa serikali nalo limechangia kwa kiwango kikubwa, kwani wawekezaji wengi wa sekta binafsi wamekosa biashara kutoka serikalini. Alisema ubanaji wa matumizi ya serikali kwa kiwango kikubwa unaweza kusababisha ukuaji wa uchumi kusinyaa.
“Nadhani hapa tunatakiwa kuchukua hatua kuhakikisha kwamba tunaelekeza sera zetu kuufanya uchumi wetu upanuke sio kusinyaa, ikibidi kwa kulegeza hata ubanaji wa matumizi ya serikali,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya REPOA, Dk Donald Mmari, anaamini kwamba iwapo hali hii itaendelea, basi kuna uwezekano mkubwa wa serikali kutafuta fedha kwa ajili ya “kuchangamsha” uchumi.
Dk Mmari anasema kwamba kushuka kwa ukuaji wa mikopo kwenye sekta kama kilimo ni matokeo ya hali mbaya ya hewa ambayo imelikumba taifa katika kipindi cha miaka miwili.
“Tumekuwa na tatizo la ukame kwa muda wa miaka miwili, wakulima wengi walikwama na wengine kushindwa kurudisha mikopo. Hii imesababisha kuongezeka kwa hatari za kibiashara miongoni mwa watoa mikopo,” alisema kwenye mazungumzo ya simu na Raia Mwema.
Alisema kwamba kushuka kwa bei ya bidhaa nyingi za nje hasa za kilimo na kubadilishwa kwa sera za uchumi kwa nchi ya China, nchi ambayo ni soko kubwa la bidhaa, nayo imeongeza hatari za kibiashara.
“Wanachofanya benki ni kukabiliana na hilo kwa kuwa makini katika ukopeshaji,” alisema.
Dk Mmari amebainisha kwamba, iwapo hali hii itaendelea, kuna uwezekano wa kuongezeka kwa gharama za mikopo kwani benki nyingi zitajihami kukabiliana na hatari za kibiashara (risks).
“Kama hali hii itaendelea kwa kipindi kirefu, basi serikali ijiandae kutoa fedha kwa ajili ya kuchachua (kuchangamsha) uchumi,” alisema Dk Mmari.
Ripoti mbalimbali zimeonyesha kwamba hata urudishaji wa mikopo nao umeanza kusuasua hasa kwenye sekta za nyumba, binafsi, pamoja na viwanda.
Katika robo ya pili ya mwaka, kiwango cha ukuaji wa ujazo wa fedha (M3), ambazo ni fedha zote zilizoko kwenye mzunguko, amana za benki na akaunti za fedha za kigeni, kimeshuka na kufikia asilimia 12.5 mwezi Juni mwaka huu kutoka asilimia 13.1 kwa mwezi Juni, mwaka 2015.
Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa ujazo wa fedha inatokana na kupungua kwa rasilimali za kigeni kwenye sekta ya benki, kupungua kwa utoaji wa mikopo na kupungua kwa uwekaji wa akiba kwa raia wa kigeni.
Ripoti ya mapitio ya uchumi ya mwezi Juni pia imeonyesha kwamba kasi ya ukuaji wa mikopo kwenye sekta binafsi za uzalishaji imepungua hadi kufikia asilimia 19.1 mwezi Juni mwaka huu kutoka asilimia 23.6 kwenye robo iliyoishia mwezi Machi mwaka huu.
Sekta nyingine zilizokumbwa na kupungua kwa huduma za mikopo kwa mujibu wa benki kuu ni biashara ambapo ukuaji umeshuka hadi kufikia asilimia 8.7 mwezi Agosti mwaka huu kutoka asilimia 14.7 mwezi Agosti mwaka jana.
Ukuaji wa mikopo kwenye sekta ya mawasiliano nao uliporomoka kutoka asilimia 28.4 mwezi Agosti mwaka jana hadi asilimia 9.3 Agosti mwaka huu na sekta ya hoteli nayo ikishuka kutoka asilimia 33.6 hadi asilimia 0.3 katika kipindi hicho hicho.
Sekta ambayo bado benki zina imani nayo katika utoaji wa mikopo ni mikopo ya binafsi (personal loans), kwani kasi ya ukuaji wake iliongezeka hadi kufikia asilimia 36.7 mwezi Juni mwaka huu, kutoka asilimia 24.9 mwezi Agosti mwaka jana.
Hata hivyo, pamoja na kuporomoka kwa ukuaji wa mikopo, viwango vya riba kwenye utoaji wa mikopo katika kipindi hicho haukubadilika kwa kiasi kikubwa kwani kiwango cha ukopeshaji cha wastani kimebakia asilimia 16.